Uzinduzi Wa Taasisi Ya Taaluma Za Kiswahili, 27/06/2009
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili [TATAKI] itazinduliwa tarehe 27/06/2009. Taasisi hii mpya ni tokeo la muungano wa Idara ya Kiswahili iliyokuwa zamani chini ya Kitivo cha Fani na Sayansi za Jamii na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili [TUKI].
Taasisi hii mpya itakuwa na majukumu makuu matatu. Jukumu la kwanza ni kufundisha wataalamu wa viwango mbalimbali vya shahada kwa lengo la kukuza taaluma ya Kiswahili na kueneza Kiswahili Afrika Mashariki na duniani kote. Jukumu la pili litakuwa ni kufanya utafiti katika nyanja zote za lugha ya Kiswahili zikiwemo Isimu, Fasihi, teknolojia ya lugha na Utamaduni. Jukumu la tatu litakuwa ni kutoa ushauri wa kitaalamu kwa umma, vyombo vya serikali, mashirika ya ndani na nje ya nchi.
Ili kutekeleza majukumu yake ya ufundishaji, Taasisi itakuwa na Idara za ufundishaji mbili: Idara ya Lugha ya Kiswahili na Isimu na Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji. Idara hizo zitaendesha programu za shahada ya kwanza, uzamili (shahada ya pili), na uzamivu (shahada ya tatu).
Taasisi hiyo mpya itakuwa pia na vituo vine vya utafiti: Kituo cha Leksikografia; Kituo cha Istilahi, Tafsiri, Ukalimani na Teknolojia ya Lugha; Kituo cha Kiswahili kwa Wageni; na Kituo cha Mapokeo-simulizi ya Kiswahili na Kiafrika. Kwa upande wa huduma kwa umma, taasisi itafanya kazi za ukalimani, tafsiri, kusoma miswada mbalimbali na kuendesha kozi fupifupi za uandishi, ukalimani na uhariri.
Shughuli za uzinduzi zitaanza saa saba mchana kwa maandamano kuanzia Jengo la Kiswahili hadi Ukumbi wa Nkrumah na kuisha saa 12 jioni. Kutokana na umuhimu wa Taasisi hii kwa Taifa na Chuo Kikuu, mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Imetolewa na Mkurugenzi,
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili


